Family Benevolence Fund (FBF)
MEMBER REGISTRATION FORM
Mpango huu wa mfuko umeundwa kwa ajili ya kuwasaidia wanachama wa FAMILY kukabiliana na mzigo wa kifedha unaotokana na matukio ya kijamii. Kwa maelezo zaidi bonyeza hapa.
Kusudi
Mpango huu wa mfuko umeundwa kwa ajili ya kuwasaidia wanachama wa FAMILY kukabiliana na mzigo wa kifedha unaotokana na matukio ya kijamii (kufiwa, harusi, send-off, ajali, majanga ya asili, magonjwa ya muda mrefu yasiyo ya kuambukizwa). Huenda usigharamie gharama zote lakini umekusudia kupunguza mzigo wa kifedha kwa mwanafamilia.
Wigo wa Mpango:
Wana-familia watakaohudumiwa na mfuko: Mwanachama wa FAMILY (Mwanafamilia) na wategemezi wake ambao ni mwenzi, watoto, na wazazi tu.
Msaada wa Kifedha:
Kiasi cha sasa cha kulipwa kwa mwanachama endapo atapatwa na mojawapo ya mambo tajwa hapo juu atachangiwa Tshs 2,500,000 kutoka kwenye mfuko, na kwa wategemezi mwanachama atachangiwa Tshs 1,500,000. Kwa Harusi/send-off kiasi cha Tzs 1,000,000 kwa mwanachama, na Tzs 700,000 kwa wategemezi/watoto, kulingana na vigezo vilivyowekwa.
Usajili:
Ada ya usajili ya mara moja ambayo haiwezi kurejeshwa ni Tshs 200,000 kwa kila mwanachama. Kila mwanachama atatakiwa kujisajili kwa kutumia fomu iliyoambatanishwa. Kwa wanandoa, kila mwanandoa atatakiwa kujiandikisha kama mwanachama binafsi na kila mmoja atalipa Tshs 200,000 kwa mwaka, kiasi ambacho kitatolewa si zaidi ya mara 4 katika mwaka husika (kila miezi mitatu angalau elf 50).
Mchango wa Kutunisha Mfuko:
Kufuatia utoaji wa fedha kwa mwanachama, mfuko utakuwa ukijazwa kwa mchango wa pamoja ili kufidia jumla ya fedha zilizotolewa kwa wanachama kwa mwaka uliopita. Mchango huu utakamilika ndani ya miezi mitatu (siku 90). mwanachama atatakiwa kuchangia Tshs 50,000 kwa ajili ya kutunisha mfuko wa familia.
Tunasaidia masuala ya jamii na kufanya kazi ya Mungu kwa mafanikio zaidi!
Jisajili Hapa
- Ikiwa atajiunga mmojawapo wa wanandoa, litakapotokea moja ya uhitaji tajwa hapo juu katika familia, atahudumiwa na mfuko kama mwanachama mmoja kulingana na utaratibu wa mfuko.
- Ikiwa watajiunga mume na mke, litakapotokea tatizo katika familia, kila mmoja atahudumiwa na mfukokama mwanachama anayejitegemea kwa kuwa kila mmoja ni mchangiaji katika mfuko.
Baada ya mfuko kuanza kufanya kazi, usajili wa wanachama wapya utafanyika wakati wowote.
Baada ya mwanachama kukidhi vigezo vya usajili, mwanachama mpya atasubiri muda ya siku 90 kabla uanachama wake kuwa HAI na kuanza kupokea fedha kutoka kwenye mfuko.
Sheria na kanuni za mpango huu zinaweza kubadilika kulingana na wakati na uanachama wa mfuko kukua ili kuruhusu wanachama kutumia kikamilifu manufaa yanayotolewa na mpango huu. Uongozi wa FAMILY kwa kushirikiana na wanachama unaweza kufanya mabadiliko inapobidi.
Taratibu za kutunisha mfuko baada ya pesa kutolewa kwa mwanachama
Iwapo mwanachama hatatoa mchango ndani ya muda husika (siku 90 za kwanza), basi atasimamishwa hapo hapo kwa siku 30 na HATATAKIWA kupokea fedha yoyote endapo atapata mambo tajwa hapo juu ndani ya hizo siku 30.
Ikiwa mwanachama aliyesimamishwa atalipa deni lake kikamilifu ndani ya siku 30 za kusimamishwa, atarejeshwa kwenye mfuko baada ya siku 30 tangu tarehe ya malipo ya fedha ilipotolewa.
Ikiwa mwanachama hatachangia kufikia tarehe ya mwisho iliyotajwa (siku 90), na bado hajachangia ndani ya siku 30 baada ya tarehe ya mwisho uanachama wake utasitishwa. Na kama atapenda kurudi basi atafuata utaratibu wa usajili kama mwanachama mpya.
Mwanachama atahesabiwa kuwa anakidhi vigezo vya kuchangiwa endapo amechangia angalau asilimia 75 ya ada ya kiingilio, mchango wa Tshs 50,000 wa kutunisha mfuko kila mwaka pamoja na kurudisha kiasi kilichochangiwa kwa mwaka uliopita.
Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQs)
Ni kiasi gani cha kiingilio kinachotakiwa?
Kila mwanachama anatakiwa kuchangia kiingilio cha Tzs 200,000.
Je, kuna utaratibu gani wa kutoa mchango?
Mchango wa Tzs 200,000 unapaswa kutolewa mara moja. Hata hivyo, kutokana na hali za kiuchumi, tumetoa wigo wa kutoa mara nne kwa mwaka, yaani kila robo mwaka angalau Tzs 50,000. NB: Robo mwaka ni miezi mitatu.
Mfuko utasaidiaje wanachama katika matukio ya kijamii?
Kama kutakuwa na uhitaji wa jambo la kijamii, iwe la furaha au huzuni, tutatoa sadaka ya upendo kutoka kwenye mfuko kiasi cha Tzs 1,500,000 au Tzs 2,500,000.
Kwa Harusi/send-off kiasi cha Tzs 1,000,000 kwa mwanachama, na Tzs 700,000 kwa wategemezi/watoto, kulingana na vigezo vilivyowekwa
Tuna uzoefu gani kuhusu matukio ya kijamii?
Tunamshukuru Mungu kwamba ametulinda kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita ya uhai wa kundi hili la Family, na hatujapata kuwa na matukio zaidi ya manne kwa mwaka. Matukio hayo yanaweza kutokea kwa nyakati mbalimbali, hivyo tumejipanga kutiana moyo na kuonesha ushirika wetu. Mara zote tumekuwa tukichangishana pindi tukio linapotokea jambo ambalo limekuwa na changamoto mbalimbali za ukusanyaji, viwango n.k; Mfuko huu umekusudia kutatua hizo changamoto.
Kwa wastani, ni kiasi gani kinachotolewa kwa mwaka?
Kwa wastani, tunatarajia kutoa Tzs 6,000,000 kwa mwaka kutokana na uzoefu wa miaka iliyopita.
Je, lengo na matumizi ya mfuko ni yapi?
Mfuko huu sio chama cha kufa na kuzikana wala sio wa maafa pekee. Tumependekeza matumizi mengine kulingana na lengo na kusudi la Familia.
Itakuwaje matumizi ya fedha za mwishoni mwa mwaka ambazo hazijatumika?
Ifikapo mwisho wa mwaka, ambapo kila mwanachama atakuwa ametoa mchango wa Tzs 200,000, fedha ambazo hazijatumika kwenye mambo ya kijamii zitapangiwa majukumu mengine, maana huu sio mfuko wa kukaa na pesa kusubiri matukio.
Mchango wa kutunisha mfuko: Je, baada ya kutoa mchango wa Tsh. 200,000/= kila mwanachama atapaswa kuchangia tena?
Ndio! Kila mwanachama atachangia TZS 50,000 kila mwaka kuendeleza mfuko wetu na kurejesha kiasi kilichotumika mwaka uliopita. Kila mwaka kuna mtiririko wa matukio kuhusu shughuli za mfuko, na wanachama wanatarajiwa kuendelea kuchangia 50k ya kila mwaka pamoja na kurejesha sehemu ya fedha iliyotumika mwaka uliotangulia.
Mfuko hubaki na kiasi gani kwa mgawanyo wa faida?
Kwa mfano, ikiwa jumla ya mapato ni milioni 20, baada ya kutekeleza matukio ya kijamii kwa milioni 6, kiasi kinachobaki cha milioni 14 ndicho kitagawanywa katika asilimia 40 kwa kazi ya Mungu, asilimia 40 kwa uwekezaji, na asilimia 20 kwa akiba.
Je, mchango wa Mkutano wa Injili unahusishwa?
Hapana, mchango wa Mkutano wa Injili ni tofauti na utaendelea kama kawaida, kulingana na bajeti ya mwaka huo na mahali ptakapochaguliwa!
Kazi ya Mungu inahusisha nini?
Kazi ya Mungu haimaanishi Mkutano wa Injili pekee; inajumuisha shughuli nyingine za kujenga Ufalme wa Mungu kama ununuzi wa viti, ujenzi wa Kanisa, na kuwezesha usafiri wa wachungaji waliko kwenye mazingira magumu.
Je, FBF ni kundi dogo ndani ya Family?
Hapana, FBF (Family Benevolence Fund) ni mfuko wa kundi linaloitwa Family. Hili sio kundi dogo; ni sehemu muhimu ya Family.
Nini msingi wa utaratibu wa michango na matumizi?
Msingi ni kutengeneza, kuratibu, na kurasimisha utaratibu wa michango na matumizi yenye tija kwa lengo na kusudi la Family, kudumisha ushirika na utumishi wa Kazi ya Mungu.
Je, mgawanyo wa 40:40:20 unafanyika lini?
Mgawanyo wa 40:40:20 unafanyika kila mwisho wa mwaka, baada ya matumizi kufanyika kwa mwaka husika, kwa pesa zilizobaki.
Matumizi ya 40% kwenye Kazi ya Mungu katika mfuko yatatumika vipi?
Hii asilimia inatumika kusaidia Kazi ya Mungu, hasa kwenye maeneo yenye uhitaji. Tunaanza na watumishi wenzetu ambao ni wanachama katika Family hii, kisha wengineo kulingana na uhitaji. Mfuko ukiwa na wanachama 100, hii itakuwa kati ya TZS 5.6M – 8M.
Matumizi ya 40% kwenye Uwekezaji wa Muda Mrefu: Kwanini tunawekeza 40% ya mfuko?
Hii itatumika kwa uwekezaji wa muda mrefu/kati, mf. katika hati fungani au UTT ambazo hutoa riba kila miezi 6. Riba hii inaweza kuendeleza mfuko kupitia uwekezaji zaidi. Mfano wa matumizi makubwa yajayo ni kununua SET YA VYOMBO+ JUKWAA NA GARI LA INJILI.
Kwanini tunaweka 20% ya mfuko kama Akiba?
Tunabakisha asilimia hii kama akiba anzia kila mwaka mpya, yenye wastani wa TZS 2.8M-4M. Inatumika kuweka usalama kwa masuala ya kijamii yanayoweza kutokea kati ya Januari na Machi.
Je utekelezaji unaanza lini?
Utekelezaji unaanza sasa, tutakuwa na fomu ya kujisajili ambapo mwanachama atajaza fomu ili tuweze kuhifadhi taarifa zake, na kisha kutoa mchango wake.
Utaratibu wa kutoa/kukusanya michango ukoje?
Michango inakusanywa kupitia akaunti ya M-KOBA iitwayo UDOM FAMILY kama hujaunganishwa bado tafadhali wasiliana na viongozi.
Mwisho wa kujiunga na mfuko ni lini?
Mwanachama atahesabika kuwa amejiunga/amejisajili baada ya kujaza taarifa zake kwenye mfumo na kuchangia angalau Tsh elfu 50 mwishoni mwa mwa mwezi wa Machi 2025.
Uongozi wa FBF:
Mwenyekiti: John Massenza
Katibu: Yusuph Jengela
Mweka Hazina: Anna Danda